Siku
tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa tamko la Jukwaa la Wakristo (TCF)
kuwataka waumini wao kupigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa lilikuwa
la hasira, viongozi hao wamejitokeza tena na kusisitiza kwamba msimamo wao huo
utabaki kama ulivyo.
Katika tamko pamoja walilolitoa jana
baada ya kukutana juzi mjini Dodoma, viongozi hao wamemtahadharisha Rais
Kikwete kuwa kuendelea kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama
ya Kadhi, kunaweza kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo
Serikali ndiyo itakayolaumiwa.
Tamko hilo limesainiwa na viongozi
walewale waliosaini lile la awali la Machi 12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa
Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu
Daniel Awet.
Tamko hilo la maneno 921, limeendelea
kuwataka waumini wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa
kwa kupiga kura ya ‘hapana,’ msimamo ambao tayari umeibua msuguano baina yao na
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo aliyesema viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini wao aina
ya kura wanayostahili kupiga.
Pia, Jukwaa hilo limewataka viongozi
wakuu wa Serikali –Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete wasifurahi kwamba
ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini waliozungumza nao hivi karibuni, kwa
kuwa watu waliokutana nao si wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa uamuzi
au kukubaliana juu ya jambo la kitaifa.
“Maaskofu tuliokutana hapa (mjini
Dodoma) hatuna hasira na wala hatuongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia
maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri, tunafikia maamuzi
yetu baada ya maombi na sala na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga
Taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano,” lilisema tamko hilo
likihitimishwa kwa maneno ya Biblia kutoka Mithali 29: 1, “Aonywaye mara nyingi
akishupaza shingo, atavunjika ghafla, wala hapati dawa.”
Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete
akifungua mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha
wajumbe kutoka mikoa mbalimbali ikijumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na
Kikristo, alisema msimamo wa TCF kuhusu kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba
Inayopendekezwa ni wa hasira na usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.
“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa
umakini, imenishangaza, imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini
wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema: “Waacheni waumini
waamue Katiba wanayoitaka wao... hayo matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa
Serikali kupeleka bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi.”
Maaskofu hao walikuwa Dodoma kufuatilia
kwa kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2014
unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la
Sheria za Kiislamu la mwaka 1964 unaotambua Mahakama ya Kadhi.
“Muswada huu unapendekeza kuanzishwa
Mahakama ya Kadhi ambao utawasilishwa bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo
kuufanya umma wa Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo
wakati bado hoja zetu za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria
ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa,” Ilieleza taarifa hiyo.
“Tunamtaka Rais aagize muswada huu
uondolewe bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa utafiti wa Tume ya kurekebisha
sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi. Vinginevyo,
kuendelea kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba Serikali inajihusisha
na itagharimia mahakama hiyo.”
Post a Comment