Dar es Salaam. Utata umeibuka kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo
wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada
ya kiongozi huyo kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
Gwajima
aliyetolewa kwenye chumba cha uangalizi maalumu cha Hospitali ya TMJ jana,
amelitaka Jeshi la Polisi kurudisha bastola hiyo, akisema ni mali na aliiagiza
ipelekwe hospitalini kwa sababu ya kujilinda.
Akizungumza
na waandishi wa habari hospitalini hapo alipolazwa baada ya kuishiwa nguvu na
kupoteza fahamu akiwa katika mahojiano na polisi, Gwajima alisema anashangaa
kukamatwa kwa wachungaji wake waliokuwapo kwa ajili ya kumlinda.
Hata hivyo,
katika kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema bunduki hiyo haina umiliki halali wa Gwajima wala wa
wachungaji 15 waliokamatwa lakini baadaye jioni baada ya maelezo ya Gwajima,
alitoa taarifa akisema bastola hiyo ni mali halali ya askofu huyo. Pia alisema
kuhusu risasi 17 za bunduki aina ya Shortgun, Gwajima anamiliki bunduki ya aina
hiyo lakini akasema uchunguzi kuhusu watu hao 15 unaendelea.
Kauli ya Gwajima
Akizungumza
kwa shida akiwa amejishika tumbo, Gwajima alisema alipopata taarifa za uvumi
kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki dunia, aliagiza wachungaji waende
hospitalini kwa ajili ya kumlinda, lakini wakaishia mikononi mwa polisi
wakidaiwa kutaka kumtorosha.
Alisema
alihofia kuwapo kwa watu wabaya ambao wangeweza kumdhuru halafu wakasingizia
kitendo hicho kufanywa na polisi kwa kuwa alipata tatizo akiwa mikononi mwao.
“Usiku
wasiwasi ulizidi, huku kila mmoja akiwa hafahamu kwa nini ujumbe wa namna ile
unasambazwa kwenye mitandao, msambazaji ni nani, ana nia gani, nikaamua
kuwaagiza waniletee silaha yangu iliyokuwa kwenye begi ili likitokea lolote
niweze kujilinda,” alisema Gwajima.
Alisema
alishangaa kukamatwa wachungaji wake na kuchukua silaha iliyokuwa ndani ya begi
na hadi jana hakuwa ameulizwa chochote kuhusu umiliki wa silaha hiyo.
“Kabla
sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa kinachodaiwa kuwa nilitaka
kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka kuzungumza na ZCO (Mkuu wa Upelelezi
Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi ya ile silaha ninayo,” alisema Gwajima.
Alisema
madai kuwa alitaka kutoroka ilihali polisi alikwenda mwenyewe akitokea Arusha
baada ya kusoma katika vyombo vya habari kuwa anatafutwa.
Alifafanua
kuwa hata alipofika polisi kwa ajili ya mahojiano hakuwa na shaka hata kidogo,
lakini alishangaa kuona anaishiwa nguvu kila baada ya muda na alipoona kichwa
kinamuuma, akawaomba wampeleke hospitali ili mambo mengine yafuate baadaye,
kitu ambacho hakikufanyika kwa wakati.
Post a Comment