Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwazuia wananchi
kwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
mwaka huu ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mkono.
Lowassa alitoa kauli hiyo nyumbani kwake mjini Dodoma jana
wakati alipotembelewa na kundi jipya kutoka Mbarali mkoani Mbeya waliokwenda
kumshawishi atangaze nia kugombea urais.
Lowassa ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kusema kuwa kwa kuandaa makundi ya kumshawishi,
mbunge huyo wa Monduli anajua adhabu yake na anaweza kupoteza sifa za kuwa
mgombea urais kupitia CCM.
“Sasa mmekuja siku mbaya kwa sababu jana kuna watu wamesema
maneno mengi mabaya ambayo kwa malezi yangu mimi mambo ya chama humalizwa
kwenye vikao vya chama na siyo kwenye vyombo vya habari. Mnazungumza,
mnaelewana mnatoka pale,” alisema.
“Na utaratibu huu ulioanzishwa na watu, mimi ni vigumu kuuzuia,
utazuiaje mafuriko kwa mikono? Mafuriko yanakuja halafu nazuia kwa mikono
nitaweza kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia,” alisema.
Mambo ya chama
Lowassa ambaye hivi karibuni aliweka bayana kuwa ameshawishika
kuwania nafasi hiyo, alisema, “Lakini mambo ya chama hayawezi kuwa kwenye
ma-TV, magazeti na maredio, mara huyu hivi, mara huyu vipi. Mkiona chama
kinakwenda kwa utaratibu huo, ni hatari sana, CCM ninayoijua mimi ni ya vikao.”
Alisema hakusudii kujibu hizo hoja (za Nape) bali rafiki yake
Hussein Bashe amezielezea vizuri.
“Niseme mawili tu yanayonisikitisha wanasema eti nawaiteni,
nakupeni fedha, mimi hela natoa wapi? Lakini kibaya zaidi nikiweka maturubai
hapa ni kosa, mkiwa na viti hapa ni makosa? Na wanasema nawapeni chakula mambo
ya ajabu sana na yanasemwa na watu wazima wenye heshima
zao,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Juzi walikuwapo vijana 300 hapa, nitawapikia chakula
nitawaweza? Nyie kwa wingi huu mtaenea hapa? Lakini ni vibaya unamdhalilisha
binadamu mwenzako kuwa maisha yake yote ni kufikiria tumbo. Hamna cha kufikiri
isipokuwa tumbo, kwa hiyo mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowassa awapeni
chakula, ni kudhalilisha watu.”
Alisema watu wanaofika nyumbani kwake wanafanya hivyo kwa
utashi, hiari na gharama zao wenyewe na wengine yeye hawafahamu kabisa.
Post a Comment