Dar/Mbeya.
Wakati viongozi wa vyama vya upinzani wakieleza hofu ya Uchaguzi Mkuu
kuahirishwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesitisha mchakato wa
kuandikisha wapigakura mkoani Mbeya uliopangwa kufanyika kuanzia Mei 5 hadi
itakapotangazwa tena.
Tayari kazi
hiyo inaendelea kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa ambako kazi
hiyo pia ilianza kwa kusuasua, na NEC ilitarajiwa kuongeza kasi ya uandikishaji
kwa kuingia mikoa ya Dodoma, Katavi na Mbeya ambako mpango huo umesitishwa kwa
muda usiojulikana.
Akizungumza
na gazeti hili jana, kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Dk Lazaro Samweli alisema
walipewa taarifa za kusitisha uandikishaji hadi hapo watapotaarifiwa tena licha
ya Tume hiyo kupeleka vifaa vya BVR.
Mwezi
uliopita, Nec ilitangaza kwamba ingeanza kazi hiyo ya kuboresha Daftari la
Wapigakura mkoani hapa Mei 5, jambo ambalo lilisababisha uongozi wa jiji
utangaze nafasi za kazi ya kuandikisha kwa wenye ujuzi wa kompyuta.
“Kabla ya
Mei 4, ofisa kutoka Tume ya Uchaguzi alikuja akatuambia tusimamishe
mchakato wa kuwapata watu wa kusimamia hadi hapo tutakapotaarifiwa, lakini
vifaa tulishavipokea, hivyo tunawasubiri wao watakavyotuelekeza taratibu zao
kwa mara nyingine tena,” alisema Dk Samweli.
Alisema
walipokea mashine 86 za BVR kutoka NEC na kwamba mashine 15 kati ya hizo ni kwa
ajili ya mafunzo ya waandikishaji na 71 zinazosalia zitakuwa maalumu kwa kazi
yenyewe ya kuandikishia.
Viongozi wa
vyama vya upinzani wamekuwa wakituhumu kuwa kusuasua huko kwa kazi ya kuboresha
Daftari la Wapigakura ni mpango wa kutaka Serikali ya Awamu ya Nne iongezewa
muda kwa kuwa haijajiandaa kukabidhi madaraka.
Wanajenga
hoja hizo kwa kueleza kuwa hadi sasa Serikali haijatoa zabuni ya ununuzi wa
vifaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, wakati haitakuwa rahisi kukamilisha
uandikishaji wapigakura mapema baada ya kazi hiyo kuchukua muda mrefu mkoani
Njombe na uchache wa vifaa.
Mwenyekiti
wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hakuwa na taarifa za kusitishwa kwa
uandikishaji mkoani Mbeya, lakini akaongeza kuwa wananchi wanatakiwa kuwa
wavumilivu kwani uandikishaji utafanyika kama ulilovyopangwa.
“Unajua
sikuwa na taarifa hizo kwa sababu nilikuwa katika kikao na wenyeviti wenzangu
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kama kweli
limesitishwa, itakuwa ni mchakato mdogo wa maandalizi haujakamilika. Ila
niwatoe hofu wakazi wa mkoa huo uandikishaji utafanyika kama ulivyopangwa,”
alisema Jaji Lubuva.
“Unaweza
kuwa na vifaa lakini kukawa na mambo madogo madogo yanayokwamisha na ndicho
kilichotokea Mbeya japokuwa sina taarifa kamili za kusitisha mchakato huu,”
alisisitiza Jaji Lubuva.
Post a Comment