Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif
Hamad ametoa tuhuma nzito dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) akidai kuwa
iliandikisha na kuruhusu wapigakura wasiostahili zaidi ya 10,000 kupiga kura
katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, wakiwamo marehemu 8,507.
Maalim Seif
aliyewania urais wa Zanzibar katika uchaguzi huo na kushindwa ikiwa ni mara ya
tano na wagombea wa CCM, alitoa tuhuma hizo jana alipozungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam akisema wapigakura hao wasiostahili, bado wapo
kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura la Zanzibar.
Maalim Seif
ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alikuwa akizungumzia utafiti wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura kwa Zanzibar uliofanywa kati ya Agosti 2014 hadi Machi
2015. Alieleza pia kwa nini hakulalamika wakati huo na badala yake akakubali
matokeo.
Kwa nini
alikubali matokeo?
“Ni ukweli
usiopingika kwamba uchaguzi huo ulikuwa na mapungufu lukuki lakini mawakala
wetu hawakuwa na vithibitisho, hatukuweza kupinga matokeo yale kwa sababu
hatukuwa na uthibitisho wowote.”
Aliongeza,
“Hivi unaweza kusema matokeo siyo ya haki wakati huna uthibitisho? Lakini
utafiti huu umeweka wazi mambo yote yaliyofanywa nyuma ya pazia kwenye uchaguzi
uliopita, kwa hiyo sasa tuna uthibitisho wa kutosha.”
Kiongozi
huyo alisema endapo kasoro hizo zikifanyiwa kazi, Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed
Shein ajiandae kisaikolojia kuwa makamu wa rais wakati yeye akiwa Rais baada ya
uchaguzi ujao.
Kasoro za uandikishaji
Kwa mujibu
utafiti huo, ZEC iliandikisha katika daftari hilo wapigakura wenye umri chini
ya miaka 18, ambao si wakazi katika maeneo waliojiandikisha na waliotumia
majina na picha ambazo siyo zao.
Alisema
licha ya baadhi ya watu hao kuwa marehemu na wengine wasiokuwa na sifa, bado
hawajafutwa kwenye daftari hilo tangu 2010 na majina yao yatatumika kupiga kura
mwaka huu.
Akizungumza
kwa kujiamini huku akitabasamu, Maalim Seif alisema utafiti huo unaonyesha kuwa
kuna zaidi ya watu 10,000 ambao waliandikishwa kinyume na sheria na kwamba
walipiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Akitoa mfano
huku akirejea utafiti huo, Maalim Seif alidai kwamba katika Jimbo la Donge, ZEC
iliandikisha watoto 463 ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 na kwamba walipiga
kura.
Source mwananchi.
Post a Comment